NGUVU YA FURSA KATIKA BIASHARA.
Moja kati ya eneo nyeti katika masuala ya biashara ni maamuzi yanafanyika juu ya kila fursa inayokuja. Matumizi ya fursa yanaweza kustawisha biashara yako kwa kiwango cha juu sana kuliko jinsi ambavyo unaweza kufikiri.
Biashara ili iweze kuwepo lazima kuwepo na fursa ya kiabiashara, hakuna biashara kama hakuna fursa ya kibiashara hivyo kila mjasiriamali ni vema akajifunza vizuri juu ya nguvu iliyopo katika fursa.
Fursa ni mazingira rafiki kwaajili ya kufanya jambo fulani.
Kama mjasiriamali ni vema ukatazama kila fursa katika jicho la biashara kwasababu mtazamo wa kibiashara (business mentality) ndiyo inayopelekea kuona fursa katika nyakati zote na katika kila hali.
Aina mbalimbali ya fursa.
I) Fursa ya kutumia muda.
Namna unavyotumia muda wako inaweza kukusaidia kujiingizia kipato au kuongeza uwezo wako ( increase your ability) katika masuala ya biashara. Muda unaweza kukusaidia jinsi ya kutumia rasimali watu mfano wafanyakazi wako wafanye kazi masaa mangapi ili kuzalisha kiwango cha bidhaa unazotaka. Muda unatoa fursa ya kutengeza aina fulani ya bidhaa kulingana na uhitaji wa soko kwa wakati huo (current demand ).
II) Fursa ya kiuchumi/ Biashara.
Katika maisha kuna fursa za kiuchumi nyingi mfano uwepo wa taasisi za kifedha unatoa fursa ya kupata mitaji ya biashara, kuwepo wa malighafi fulani kunatoa fursa ya kiabiashara, uwepo wa changamoto katika jamii unatoa fursa nyingi za kibiashara, maendeleo ya technolojia yanatoa fursa ya kuboresha bidhaa na kujitangaza ili kuongeza soko, uwepo wa mitandao ya kijamii unatoa fursa ya kutangaza baishara yako.
III) Fursa ya kimahusiano.
Ukitazama aina ya watu unaohusiana nao katika maisha yako utagundua kuna fursa ambayo inaweza kubadilisha biashara yako na maisha yako kwa ujumla, kuna watu wamepata wazo la kuanzisha biashara baada ya kutumia fursa ya kimahusiano vizuri, kuna watu wamepata mitaji ya biashara baada ya kutumia fursa ya kimahusiano, kuna watu ambao wamepata soko la bidhaa zao baada ya kutumia fursa ya kimahusiano vizuri.
IV) Fursa ya kielimu.
Kila elimu ina fursa zake lakini mara nyingi katika jamii tunayoishi kuna upande mmoja tu ndio umekuwa ukitazamwa nao ni upande wa kuajiriwa kumbe kuna upande wa kujiajiri pia. Unaweza kuanzisha kampuni inayotoa ushauri wa kitaalaumu ( Consultation Company) kulingana na taaluma uliyonayo mfano kama unaelimu ya sheria unaweza kuanzisha kampuni itakayotoa ushauri wa kisheria, kama unaelimu ya uasibu unaweza kuanzisha kampuni itakayotoa ushauri wa kifedha na masuala ya kodi, kama unaelimu ya saikolojia unaweza kutoa ushauri wa kisaikolojia na kujitengenezea kipato kizuri tu
V) Fursa ya kipaji.
Kipaji ni uwezo wa kufanya jambo fulani ambao mtu huzaliwa nao.
Kila mtu anao uwezo kufanya jambo fulani ambao amezaliwa nao mfano
Kuna mtu anauwezo mkubwa wa kuandika,
Kuna mtu anao uwezo mzuri wa kuimba,
Kuna mtu anao uwezo mzuri wa kushauri,
Kuna mtu anao uwezo mzuri wa kuongea na halaiki ya watu,
Kuna mtu anaouwezo mzuri wa kupamba, kuna mtu anao uwezo mzuri wa kupika.
Kila uwezo ambao Mungu amempa mtu unatoa fursa ya kujitengenezea kipato na kuboresha maisha yake. Ukifanikiwa kujua unakipaji cha aina gani utaweza kuangalia namna ya kufanya ili uweze kutengeneza kipato kupitia hicho kipaji
Tofauti kati ya mtu aliyefanikiwa na mtu ambaye hajafanikiwa imegawanyika katika sehemu kuu mbili.
I) Kutambua fursa.
Utambuzi wa fursa za kiabishara ni suala muhimu katika maisha ya mwanadamu ili aweze kuisha maisha yenye tija. Kuna aina ya watu ambao huona fursa kwenye kila hali na katika mazingira yoyote, watu hawa ni watu wenye mtazamo chanya juu ya changamoto zinawakabili wao na jamii kwa ujumla.
Mtu mwenye kuweza kutambua fursa za kiabishara ndiye mtu ambaye anaweza kupanga namna ya kutumia vizuri rasimali muda, fedha na hata rasimali watu.
II) Kutumia fursa.
Ukishakutambua fursa jambo muhimu ni kutumia hiyo fursa, fursa inaweza kuleta matokeo pale itakapotumia ipasavyo. Ukitaka kuona kufanikiwa katika maisha yako jifunze kutumia vizuri kila fursa unayoipata.
Kiwango cha maisha kwa mtu mmoja mmoja na kwa taifa kwa ujumla ni matokea ya maamuzi tunayofanya juu ya fursa tulizo nazo katika nchi yetu. Kama tunataka kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi kwenye taifa letu ni lazima kila mjasiriamali atumie vizuri fursa za kibiashara.
Imeandaliwa na
James Albert
Nambari ya simu +255756 471 244
Barua pepe jamesalbert157@gmail.com
Comments
Post a Comment